WANANCHI WA MAENEO YA HIFADHI TANGA WANUFAIKA NA MAFUNZO YA UONGEZAJI THAMANI WA MWANI NA USIMAMIZI WA BIASHARA
WANANCHI WA MAENEO YA HIFADHI TANGA WANUFAIKA NA MAFUNZO YA UONGEZAJI THAMANI WA MWANI NA USIMAMIZI WA BIASHARA

Jumatano Novemba 18, 2026          Tanga

Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kwa kushirikiana na wakufunzi kutoka Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) wanatoa mafunzo kwa vitendo ya siku nne kwa wananchi wanaoishi ndani ya maeneo ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu Tanga. Mafunzo yameanza leo Novemba 18, 2026 katika Ukumbi wa Maktaba ya Mkoa Tanga.

Mafunzo hayo yanawalenga wanawake na vijana wanaojishughulisha na shughuli mbadala za kiuchumi katika Hifadhi ya Bahari ya Silikanti Tanga (TACMP) na Maeneo Tengefu ya Tanga. Washiriki wanapatiwa ujuzi wa kuongeza thamani ya zao la mwani kupitia uchakataji na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na mwani sambamba na utafutaji masoko na usimamizi wa biashara.

Katika mafunzo hayo, washiriki wanajifunza namna ya kuzalisha bidhaa za vipodozi zinazotokana na mwani, ikiwemo sabuni ya miche, mafuta ya mgando, losheni na mafuta ya masaji. Aidha, mafunzo yanahusisha utengenezaji wa bidhaa za chakula kama unga wa mwani, viungo vya chai vya mwani (tea masala), aiskrimu na juisi ya mwani. Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, mmoja wa wawezeshaji alieleza kuwa lengo ni kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kuongeza thamani ya mazao yao, kuboresha masoko ya bidhaa za mwani na kuongeza kipato cha kaya zao kupitia shughuli endelevu za kiuchumi.

Mafunzo haya yanawezeshwa kupitia Mradi wa Kukuza Usimamizi Endelevu wa Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe vya Bahari Tanzania, unaolenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari na kuboresha maisha ya jamii zinazotegemea uvuvi na rasilimali za baharini. Mpango huo unatarajiwa kuchochea ubunifu na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake na vijana, huku ukiendeleza juhudi za uhifadhi wa mazingira ya bahari na matumizi endelevu ya rasilimali zake.

slot gacor